emblem

Bodi ya Filamu Tanzania

Tanzania: Mandhari nzuri kwa Utayarishaji wa Filamu

Habari

WAZIRI DKT. NDUMBARO AZINDUA BODI MBILI, AZIPA JUKUMU LA KUONGEZA MAPATO


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amezindua Bodi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) na Bodi ya Bodi ya Filamu Tanzania na kuwataka Wajumbe wa Bodi hizo kuhakikisha Sekta ya Sanaa inatoa ajira za kutosha ili wadau wafaidi matunda ya kazi zao.

Waziri Dkt. Ndumbaro amesema hayo tarehe 12 Septemba, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Bodi za Taasisi hizo, zinajishughulisha na Sekta ya Sanaa nchini na kuongeza kuwa Wajumbe wa Bodi hizo ni wawakilishi wa Serikali katika Taasisi hizo.

“Wizara hii ina dhamana kubwa na Watekelezaji wa kazi zake ni Taasisi zinazosimamiwa na Bodi, kazi yenu ni kuhakikisha Taasisi mnazozisimamia zinakua kiuchumi ili kukuza Pato la Taifa na uchumi wa wadau wa Sekta yetu ya Sanaa ambayo imekua kwa asilimia 19 ” amesisitiza Waziri Dkt. Ndumbaro.

Awali akimkaribisha Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro kuzindua Bodi hizo, Naibu Waziri Mhe. Hamis Mwinjuma amewahimiza Wajumbe wa Bodi hizo kutekeleza wajibu wao ili kuleta uhalisia na utofauti wa utendaji wa kazi wa Taasisi hizo kabla ya uteuzi na baada ya kuingia madarakani.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Saidi Yakubu amesisitiza kuwa Sekta ya Sanaa nchini imekuwa na Tanzania ni ya pili Afrika ambapo inazalisha Filamu 2000 kwa mwaka sawa na wastani Filamu sita kwa siku.

Wakizungumza kuhusu uzinduzi wa Bodi hizo, Mwenyekiti wa Bodi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) Bw. Victor Tesha na Mwenyekiti wa Bodi ya Filamu Dkt. Mona Mwakalinga wamesema watahakikisha linakuwepo jukwaa ndani litakalotumika kuonesha na kusambaza kazi za Sanaa ndani na nje ya Nchi kama ilivyo majukwaa mengine na kusisitiza watasimamia kuongeza ubora katika Filamu za Tanzania ili zipate soko kubwa zaidi duniani.

Aidha, Bodi ya Bodi ya Filamu Tanzania inaundwa na Mwenyekiti Dkt. Mona Mwakalinga, Katibu Dkt. Kiagho Kilonzo, pamoja na wajumbe:-
1. Dkt. Zilpha Saul Ombijah,
2. Bw. Kenneth Davis Kasigila,
3. Bi. Leah Elias Kihimbi,
4. Bw. Salum Abdul Mchoma na
5. Bw. Jacob Steve Mbura.