emblem

Bodi ya Filamu Tanzania

Tanzania: Mandhari nzuri kwa Utayarishaji wa Filamu

Habari

VIONGOZI WA SHIRIKISHO LA FILAMU NA VYAMA WATAKIWA KUONGEZA UWAJIBIKAJI


Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo amewataka Viongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) na Vyama 9 vinavyounda Shirikisho hilo kuongeza uwajibikaji katika utendaji wa majukumu yao ili kukuza uchumi wa Taasisi wanazozisimamia.

Dkt. Kilonzo ametoa Rai hiyo Tarehe 20 Aprili, 2022 katika Kikao Kazi cha awamu ya 6 ambacho ni muendelezo wa Vikao Kazi vya kila baada ya miezi mitatu vinavyoratibiwa na Bodi ya Filamu kwa lengo la kupeana na kukumbushana majukumu ya kiutendaji kati ya Bodi, Shirikisho na Vyama.

"Kasi ya ukuaji wa Shirikisho na Vyama si ya kuridhisha sana kutokana na kukosa uwajibikaji, Viongozi wanatakiwa kuongeza uwajibika kwenye majukumu yao ili kuamsha ari ya utendaji na kukuza vyama vyao kiuchumi" Dkt. Kilonzo.

Dkt. Kilonzo alieleza kuwa, Bodi ipo tayari kusaidia Vyama kuboresha maandiko ya miradi yao ya kiuchumi (proposal), kupitia Wataalam wake ili kuipa nguvu itakayorahisisha utafutaji wa fedha.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kilonzo aliwashauri Viongozi hao kuwa na uvumilivu wakati wa utekelezaji wa majukumu kwasababu kila Kiongozi anapitia changamoto zinazoweza kukwamisha Maendeleo, hivyo wasikwamishwe na changamoto yeyote.

Pamoja na mambo mengine, Kikao hicho kiliwapitisha Viongozi hao katika miradi mbalimbali inayotekelezwa na Bodi ili kuifahamu ikiwemo:-

1. Mafunzo kwa wadau wa Filamu,
2. Jumba Changamani la Filamu (Film Complex),
3. Jarida la FILMIKA,
4. Tuzo za Filamu Tanzania 2022,
5. Kutangaza maeneo ya kupiga picha za Filamu (Maping),
6. Urasimishaji wa maeneo yasiyo rasmi ya kutazama Filamu (Vibanda Umiza),
7. Uratibu wa Utayarishaji wa Filamu za Kizalendo, na
8. Maandalizi ya Rasimu mpya ya Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza.

Kwa upande wake Raisi wa Shirikisho la Filamu Bw. Eliya Mjatta aliiomba Bodi kupitia mradi wa Mafunzo, kuwapa mafunzo ya Uongozi Viongozi hao ili kurahisisha utendaji wa majukumu yao.

Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo Bw. Twiza Mbarouk aliwakumbusha Viongozi wenzie umuhimu wa kuimarisha Vyama kwa kufuata Katiba zao ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima na kuhakikisha kila mmoja anatimiza jukumu lake.