Habari
TUMEKUBALIANA NA WAWEKEZAJI WA FILAMU KUTOKA BOLLYWOOD (INDIA) KUINUA SEKTA YA FILAMU NCHINI.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa katika Mkutano na Wadau wa Filamu na Wawekezaji kutoka nchini India, Kampuni za Trans Innova na M - Nichan Group uliofanyika Tarehe 09 Aprili, 2022 jijini Dar es Salaam.
Waziri Mchengerwa ametaja baadhi ya maeneo ya mkakati ambayo yataanza kufanyiwa kazi katika makubaliano hayo yakiwemo:-
1. Utoaji wa Mafunzo kwa Wadau wa Filamu nchini katika maeneo ya Uandishi wa Miswada, Utayarishaji, Uongozaji na Masoko ili kuongeza weledi na kuimarisha utendaji wa Wadau.
2. Ushirikiano katika Utayarishaji wa Filamu (Co- production) baina ya Tanzania na India ili kuwainua Watayarishaji wa hapa nyumbani na kuitangaza Nchi yetu.
3. Kujenga Studio kubwa za Filamu hapa nchini zenye hadhi ya Kimataifa ili kuboresha Filamu za Kitanzania.
4. Kuboresha Chuo cha Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kwa kuongeza Mitaala mbalimbali ya Sanaa itakayotoa Shahada (Degree) kwa Wahitimu wakiwemo Waigizaji na Waongozaji wa Filamu.
Katika hatua nyingine Waziri Mchengerwa ametoa rai kwa Watayarishaji wa Filamu nchini kuandaa Filamu zitakazotangaza Utanzania na Utalii wetu ambapo Filamu hizo zitadhaminiwa na Serikali.
"Fedha za udhamini wa Filamu za kuitangaza Tanzania zipo, hivyo ni wakati wenu kutayarisha kazi hizo na Serikali tutazidhamini" alisema Mhe. Mchengerwa.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo aliwaeleza Wawekezaji hao faida za kuwekeza Nchini ikiwemo ushiriki wa Serikali katika kuhakikisha usalama wa kazi husika, uwepo wa mandhari za kuvutia za upigaji picha kama Mbuga za Wanyama pamoja na uhakika wa soko kupitia Wazungumzaji wa Lugha ya Kiswahili zaidi ya milioni 200 Duniani kote.
Mkurugenzi Mkuu wa M- Nichan Group Bw. Manohar Nichan amesema watahakikisha wanaifanya Tanzania kuwa namba moja Afrika kwa Utayarishaji wa Filamu nzuri.
Naye Raisi wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) Eliya Mjatta, alimshukuru Mhe. Waziri kwa kutafuta fursa za uwekezaji katika Filamu, na amemuahidi ushirikiano ili kwa pamoja kukuza Sekta ya Filamu na Michezo ya Kuigiza Nchini.