Habari
Tasnia ya Filamu nchini kupaa Kimataifa.

Tasnia ya Filamu nchini kupaa Kimataifa.
Hayo yamesemwa Tarehe 6.11.2021 na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa alipokutana na Muigizaji nguli wa Filamu kutoka nchini India Bw. Sanjay Dutt jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo Mhe. Bashungwa alimuomba Muigizaji huyo kushiriki katika moja ya Filamu za Kitanzania ikiwa ni sehemu ya kufungua mlango wa Soko la Kimataifa kwa Watayarishaji wazawa na kuwaachia ujuzi.
Mbali na ombi hilo Mhe. Bashungwa alieleza kuwa Tarehe 10.11.2021 Bw. Sanjay Dutt atakutana na Wadau wa Filamu nchini ili kujadili fursa za kushirikiana kati ya Tanzania na India katika Sekta ya Filamu, hususan utayarishaji wa Filamu Bora zitakazokuwa na ushindani wa soko la ndani na nje ya Nchi.
Katika hatua nyingine, Waziri Bashungwa alizungumzia suala la Tanzania kuwa Mwenyeji wa Tuzo za Kimataifa za Filamu za WFF World Oscars Signature mwaka 2023, ambapo alisema tayari ameshakutana na Muandaaji wa Tuzo hizo Dkt. Fasi Khurram ili kupanga mipango ya awali ya maandalizi ya kufanyika hapa nchini.
Kwa upande wake Bw. Sanjay Dutt alimshukuru Mhe. Waziri kwa kumpokea na kumkutanisha na Wadau wa Filamu, ambapo aliahidi kushirikiana naye katika kuitangaza Tanzania Kimataifa kupitia Sekta ya Filamu.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo, ambaye alieleza kuwa Tasnia ya Filamu nchini inazidi kukuwa na Wasanii wanatakiwa kuendelea kuipa thamani Tasnia hiyo kwa kufanya kazi bora zitakazoitangaza nchini yetu.
Wasanii mbalimbali wa Filamu walihudhuria pia mkutano huo, akiwemo Raisi wa Shirikisho la Filamu Bw. Eliya Mjatta, Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Bw. Salum Mchoma 'Chiki', Shahista Alidina 'Shaykaa', Single Mtambalike 'Rich Rich', Halima Yahaya 'Davina', pamoja na wengine wengi.