Habari
SERIKALI YAPONGEZA MAFANIKIO YA FILAMU YA VUTA N’KUVUTE
Pongezi hizo zimetolewa Tarehe 7 Septemba, 2021 na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari katika tukio la kumkabidhi Bendera ya Taifa, Mtayarishaji wa Filamu kutoka Tanzania Bw. Amil Shivji, baada ya Filamu yake ya Vuta N’kuvute kuchaguliwa kushiriki katika Tamasha la Kimataifa la Filamu Toronto.
“Serikali kupitia Bodi ya Filamu tumeona hatuwezi kumuacha aende nchini Canada bila kumpongeza na kumshika mkono, ndio maana tumekutana hapa ili tumkabidhi Bendera kwasababu anakwenda kuliwakilisha Taifa la Tanzania na tunajivunia mafanikio yake,” alisema Dkt. Kilonzo.
Mtayarishaji wa Filamu hiyo Bw. Amil Shivji alieleza kuwa, Vuta N’kuvute ni Filamu iliyotokana na Kitabu cha Mwandishi Shafi Adam Shafi, ambapo ina hadithi ya mapenzi na Siasa ya miaka ya mwishoni ya Zanzibar chini ya utawala wa kikoloni wa Mwingereza. Filamu inaonesha Tamaduni za pwani za miaka ya hamsini iliyopita katika mgawanyiko wa matabaka ya ubaguzi wa rangi ambao uliwekwa na utawala wa kikoloni.
Aidha, Filamu hiyo imetengenezwa Visiwani Zanzibar katika kipindi cha miaka miwili, kwa ushirikiano kati ya Kampuni ya Kijiweni Productions (Tanzania), Kampuni ya Big World Cinema (Afrika Kusini), pamoja na Kampuni ya Niko Film (Ujerumani).
Kwa upande wake Raisi wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) Bw. Eliya Mjata aliwataka Wadau wa Filamu kumtumia Bw. Amil Shivji katika kujifunza namna ya kufanya kazi zenye ubora ili kupata Wataalam wengi watakaoleta mapinduzi katika Sekta ya Filamu nchini na kufungua milango ya Kimataifa.
Naye Muigizaji mkubwa Bw. Salim Ahmed almaarufu Gabo aliielezea Filamu hiyo kuwa ilitayarishwa kwa kuzingatia misingi ya ufanyaji kazi, hususan kufanya Usaili wa Waigizaji walioshiriki bila kujali umaarufu wa Muigizaji ili kupata Wahusika sahihi wa maeneo watakayoigiza, ambapo yeye alilazimika kusubiri kwenye foleni ya Usaili zaidi ya saa 6, kabla ya kufanya majaribio.
Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo ulitumika kuonesha kwa mara ya kwanza Kionjo (Trailer) cha Filamu hiyo, ambapo itazinduliwa na kuoneshwa Tarehe 12 Septemba, 2021 nchini Canada.


