emblem

Bodi ya Filamu Tanzania

Tanzania: Mandhari nzuri kwa Utayarishaji wa Filamu

Habari

SCREENING FILAMU YA KIMKAKATI 'NURU YA TAIFA'


Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msigwa ameongoza jopo la wataalamu wa Filamu kutazama Filamu ya Kimkakati iitwayo 'NURU YA TAIFA' kwa lengo la kuikagua na kutoa maoni ya namna sahihi ya kuiboresha kabla haijaoneshwa kwa hadhira.

Utazamaji huo umefanyika tarehe 2 Novemba, 2024 katika ukumbi wa Sinema Century Cinemax - Dar Free Market, ambapo umehudhuriwa na wataalamu mbalimbali wa Filamu pamoja na wadau kutoka Taasisi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Filamu Dkt. Mona Mwakalinga.

Filamu ya Nuru ya Taifa ni Filamu ya kwanza kuandaliwa katika mradi wa Filamu za Kimkakati ambapo inaratibiwa na kuandaliwa kwa ushirikiano wa Bodi ya Filamu, Kituo cha Televisheni cha Safari Chaneli kilicho chini ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), pamoja na Mtozi na Muongozaji wa Filamu hiyo Bw. Ignas Mkindi.

Lengo la uandaaji wa Filamu za Kimkakati ni kuandaa Filamu za KIZALENDO zitakazokuwa na maudhui ya kiutamaduni, kihistoria, na kitalii ambayo yatajikita zaidi katika kuonesha, kutangaza na kutunza historia na jiografia ya Tanzania kwa vizazi vilivyopo, vijavyo na duniani kote ili kujenga mapenzi ya Taifa letu na kuongeza ufahamu wa rasilimali zilizopo, pamoja na kubadilisha mitazamo ya jamii zetu kutoka kupenda mambo ya nchi za nje ikiwemo Tamaduni na kupenda mambo yetu.