emblem

Bodi ya Filamu Tanzania

Tanzania: Mandhari nzuri kwa Utayarishaji wa Filamu

Habari

MJADALA WA UFADHILI WA KIFEDHA KATIKA SEKTA YA SANAA NA UTAMADUNI


Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo akichangia mada katika Mdahalo wa kifedha katika Sekta ya Sanaa na Utamaduni ulioratibiwa na Taasisi ya Culture and Development East Africa (CDEA).

Pamoja na mambo mengine amefafanua masuala mbalimbali ambayo Serikali kupitia Bodi ya Filamu Tanzania inafanya katika kusaidia ukuaji wa Sekta ya Filamu nchini ikiwemo: -

1. Serikali kupitia Bodi ya Filamu kwa kushirikiana na wadau inaratibu zoezi la uandaaji wa Filamu za Kimkakati zenye malengo ya kutangaza na kuonesha kumbukumbu muhimu za Kitaifa kama vile Viongozi, Tamaduni na Historia ya Tanzania. Aidha, hadi sasa jopo la wataalamu linaendelea na uandaaji wa Filamu ya Nuru imbayo inatarajiwa kukamilika karibuni;

2. Bodi Filamu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ipo katika hatua za mwisho za mazungumzo ya uandaaji wa Tamthilia kubwa itakayooneshwa kwa muda mrefu;

3. Bodi ya Filamu kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) ipo katika hatua za mwisho za majadiliano ya uandaaji wa Filamu ya kumbukizi ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere;

4. Bodi ya Filamu inasaidia kuimarisha Taasisi za wadau ili waweze kupata mazingira rafiki ya ufanyaji kazi, mfano vyama vinavyounda Shirikisho la Filamu Tanzania, pamoja na Shirikisho hilo katika masuala mbalimbali ikiwemo kusimamia chaguzi zao;

5. Bodi ya Filamu inasaidia uanzishwaji na uratibu wa matamasha mbalimbali ya wadau wa Filamu ikiwemo Tuzo za Filamu Kigamboni, Morogoro, Iringa, n.k; na

6. Bodi ya Filamu inatoa Mafunzo ya aina mbalimbali kwa wadau wake ikiwemo mafunzo kwa vitendo, mafunzo kwa njia ya Warsha (serminar) na mafunzo kwa njia ya uchambuzi wa Filamu yanayofanyika kila wiki katika ofisi za Bodi. Hivi karibuni Serikali imesaidia kupeleka wadau wa Filamu nchini Korea kupata mafunzo ya Uandaaji wa Filamu.

Aidha, hadi sasa tayari wadau zaidi ya elfu moja (1000) wameshapatiwa mafunzo.