emblem

Bodi ya Filamu Tanzania

Tanzania: Mandhari nzuri kwa Utayarishaji wa Filamu

Habari

​Bodi ya Filamu Tanzania yaandaa mkakati mkubwa wa kurudisha hadhi ya Michezo ya Kuigiza ya Jukwaani nchini Tanzania.


Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga katika onesho la Kupinga Ukatili wa kijinsia na watoto lililofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).

Dkt. Kasiga amesema: ili kupata wasanii bora wa filamu ni lazima kuboresha Michezo ya Kuigiza ya Jukwaani ambayo ndiyo kiini cha kuwaandaa wasanii bora.

Zaidi, amepongeza waandaaji wa onesho hilo—kikundi cha Sanaa Magomamoto kwa kuja na wazo la kuelimisha jamii dhidi ya madhara ya ukatili wa kijinsia kwa watoto. Ametoa rai kwa wasanii kuandaa maonesho ya michezo ya kuigiza kwa watoto yatakayohusisha watoto wenyewe ambapo watabeba dhana zinazowagusa na kuziwasilisha mbele ya hadhira. Hili litawasaidia watoto kupata jukwaa kubwa la kusema mambo yanayowagusa kwa namna na mtazamo wao. Kwa kufanya hivyo, itawezesha jamii kuelewa matatizo ya watoto pamoja na mapendekezo ya kuyatua matatizo yao.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Kasiga amewataka wasanii kuwekeza katika kuandaa hadithi zenye kusema matatizo ya kijamii kitu ambacho kitabeba dhana kubwa ya Sanaa kwa ajili ya maendeleo ya jamii.

Kwa kuhitimisha, amewataka wasanii kuitumia Bodi ya Filamu vizuri ili kuhakikisha wanasonga mbele kitasnia katika kupata fursa ya ajira na kusaidia jamii kwa kutoa mafunzo na kuburudisha.