emblem

Bodi ya Filamu Tanzania

Tanzania: Mandhari nzuri kwa Utayarishaji wa Filamu

Habari

Kikao kazi cha pili na uongozi wa TAFF


Viongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania Tanzania (TAFF) na vyama tisa vinavyounda Shirikisho hilo, wametakiwa kuwa na maono sawa na Serikali kupitia Bodi ya Filamu hususan kuleta tija na ufanisi katika Tasnia ya Filamu nchini.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo alipokutana na Viongozi hao katika Kikao Kazi cha pili cha kupokea taarifa za utekelezaji wa majukumu katika kipindi cha miezi 3. Kikao hiki kimefanyika tarehe 30 Machi, 2021 katika ukumbi wa mkutano wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

"Viongozi kwa vile tumeamua kufanya kazi, inabidi kuwa na maono ya pamoja ikiwa ni kuleta Maisha bora kwa Wanatasnia. Zoezi hili linaweza kufanikiwa kwa kupatikana kwa Soko la filamu ambalo litategemea ubora wa kazi baada ya Wadau kujengewa uwezo wa utendaji wa kazi hizo kupitia mafunzo. Shirikisho na Vyama vinapaswa kuwa imara kupitia Katiba na Mipango Mkakati yenye kutekelezeka" alisema Dkt. Kilonzo.

Akifafanua sifa za Kiongozi katika mada ya Uongozi, Dkt. Kilonzo aliainisha moja ya sifa za Kiongozi bora ni kuwa na uwezo wa kuonesha maono chanya kwa anaowaongoza ili kurahisisha utekelezaji wa mikakati ya maendeleo katika eneo analoliongoza.

Kwa upande wake Raisi wa Shirikisho la Filamu Bw. Eliya Mjata alitoa msisitizo kwa Viongozi wa Shirikisho na Vyama kuwa na utaratibu wa kuhudhuria vikao vya kujadili namna ya utekelezaji wa majukumu yao ili kwa pamoja wawe na maelewano. Amesema Viongozi wengi huwa hawaudhurii na baadaye kuanzisha migogoro inayotokana na kutokuwa na uelewa wa msingi wa makubaliano husika.

Kikao hicho kilimalizika kwa pande zote kufikia maazimio yafuatayo:-

1. Vyama ambavyo bado havijatimiza mikakati waliojipangia, vihakikishe vinatimiza kabla ya kikao kijacho tarehe 30 Juni, 2021;

2. Vyama vihakikishe vinapata Viongozi wa Kanda ili kupata uwakilishi katika maeneo hayo na kurahisisha utekelezaji wa malengo yao; na

3. Vyama vianze kupitia upya Katiba zao ili kuboresha maeneo yenye mapungufu.