emblem

Bodi ya Filamu Tanzania

Tanzania: Mandhari nzuri kwa Utayarishaji wa Filamu

Habari

​FILAMU YA VUTA N’KUVUTE KUIWAKILISHA TANZANIA KWENYE TUZO ZA OSCARS 2022


Mwenyekiti wa Kamati maalum ya kuchagua Filamu kutoka Tanzania itakayoshiriki katika Tuzo za Oscars Dkt. Mona Mwakalinga ameitangaza Filamu ya Vuta N’kuvute kuwa ni Filamu pekee nchini iliyokidhi vigezo vya kuwasilishwa kwenye mchakato wa Tuzo za Oscars mwaka huu (za 95) kwenye kipengele cha Filamu Bora ya Kimataifa (International Features Film).

Mwenyekiti huyo amebainisha hayo Septemba 20, 2022 ambapo amevitaja baadhi ya vigezo vilivyotumika kuichagua Filamu hiyo vikiwemo;

• Filamu iwe imetayarishwa nje ya Marekani;

• Filamu iwe imeoneshwa kwenye nchi husika kwa kipindi cha kuanzia tarehe 1 Januari, 2022, hadi 30 Novemba, 2022 na ioneshwe angalau siku saba mfululizo katika kumbi za Sinema za kibiashara kwa faida ya Mtayarishaji na Muoneshaji,

• Filamu iwe na urefu kuanzia dakika 40;

• Filamu iwe imetumia lugha nyingine mbali na Kingereza kwa zaidi 50%, Ikiwa na Subtitles sahihi za Kingereza;

• Filamu iwe katika muundo wa Digital Cinema Package (DCP) kwa ubora wa angalau 2040 kwa 1080 pixels(2k);
. Filamu iwe na sauti ya kipimo cha 5.1 au 7.1, au iwe yenye Chaneli 3 za sauti (left, right & centre);

• Filamu isiwe katika PPV (Pay-Per-View) Video in Demand;
na

• Filamu isiwe kwenye Usambazaji wa DVD au kwenye intaneti.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo ambapo ametoa rai kwa wadau wa Filamu na Watanzania kwa ujumla kuungana pamoja kuiunga mkono Filamu hiyo katika mchakato wa Tuzo za Oscars, kwakuwa ni Filamu bora ambayo hadi sasa imeshiriki katika Matamasha makubwa duniani na kushinda Tuzo zaidi ya 9 ndani na nje ya Bara la Afrika.

Filamu Nne pekee ziliwasilishwa kwa Kamati hiyo ikiwemo Filamu ya ‘I REGRET’ iliyoandaliwa na Bw. Amoor Abbas, ‘MUNGU NDIYO SULUHISHO’ iliyoandaliwa na Bw. Amoor Abbas, ‘GIZA’ pia imeandaliwa na Bw. Amoor Abbas, pamoja na Filamu ya Vuta N’kuvute iliyoandaliwa na Kijiweni Productions na kuongozwa na Amil Shivji.