emblem

Bodi ya Filamu Tanzania

Tanzania: Mandhari nzuri kwa Utayarishaji wa Filamu

Habari

​FILAMU 234 ZIMEPITA KATIKA MCHUJO WA AWALI WA TUZO ZA FILAMU TANZANIA 2023


Kufuatia zoezi la ukusanyaji wa Filamu kutoka Mikoa ya Tanzania Bara, Zanzibar na Nchi za Afrika Mashariki, Bodi ya Filamu imetangaza jumla ya Filamu 234 zilizopita katika mchujo wa awali wa Tuzo za Filamu Tanzania 2023, katika hafla iliyofanyika Oktoba 31 jijini Dar es Salaam.

Jumla ya Filamu 565 zilipokelewa kwa nia ya kushiriki katika vipengele vya Tuzo za mwaka 2023 ambapo Filamu 535 zimetoka Tanzania na Filamu 30 kutoka nje ya Tanzania katika Nchi za Kenya, Uganda na DRC.

Idadi ya Filamu zilizopita mchujo wa awali ni kubwa zaidi kulinganisha na miaka ya nyuma. Mwaka Jana jumla ya Filamu 189 zilipita mchujo kati ya Filamu 840 zilizopokelewa. Mwaka huu jumla ya Filamu 204 zimekidhi vigezo katika hatua hii ya awali, kati ya Filamu 565 zilizokusanywa. Kitakwimu, mwaka huu 41% ya Filamu zilizokusanywa zimekidhi vigezo, ikiwa ni ongezeko la 18% kutoka 23% ya Filamu zilizochaguliwa mwaka jana.

Aidha, Uoneshaji wa Filamu utakuwa huru kwa Kituo chochote kitakachoweza kuonesha Filamu hizo badala ya Azam pekee kama ilivyokuwa kwa miaka iliyopita ya 2021 na 2022, ambapo kwa mwaka 2023 Filamu zitaoneshwa katika majukwaa mbalimbali ikiwemo Azam TV kupitia Chaneli ya Sinema Zetu na Televisheni Mtandao ya Airtel (Airtel Tv).

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msigwa ambapo pamoja na mambo mengine ametoa wito kwa wadau wa Filamu kuandaa Filamu za kimkakati zenye maudhui ya kuitangaza Nchi yetu, ili kupitia Filamu hizo watakuwa wanaunga mkono jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameshaonesha njia kwenye Filamu za Tanzania: The Royal Tour, pamoja na ile ya Kijiji cha Milele itakayotoka hivi karibuni.