Habari
BODI YA FILAMU YAPONGEZWA

Bodi ya Filamu Tanzania imepongezwa kwa kuendelea kuisimamia Tasnia ya Filamu kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu kwa lengo la kukuza na kuendeleza Sanaa kupitia Tasnia hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa Tarehe 10 Mei, 2022 na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sanaa Bi. Leah Kihimbi aliyeambatana na Mkurugenzi Msaidizi Maadili na Urithi wa Taifa Dkt. Julieth Kabyemela na Mkurugenzi Msaidizi Haki na Maendeleo ya Wasanii Dkt. Asha Salim kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, katika kikao cha kuwapitisha viongozi hao katika majukumu mbalimbali ikiwemo miradi inayotekelezwa na Bodi.
Pamoja na mambo mengine, Wakurugenzi hao wasaidizi walipata fursa ya kuhudhuria katika darasa maalum la kutoa Mafunzo elekezi kwa Wadau wa Filamu kupitia uchambuzi wa Filamu (Screening), ambapo Filamu ya SALIBOKO iliyoandaliwa na Kampuni ya Dollar Loss Studio ilitazamwa na kuchambuliwa kiufundi na Wataalam kutoka Bodi ya Filamu pamoja na Watendaji wa kazi hiyo (Film Crew).
Aidha, uchambuzi yakinifu ulifanyika na Wataalam walielekezwa namna bora zaidi ya utendaji kazi kwa mapungufu yaliyobainika ili kuboresha kazi zijazo.
Mafunzo haya ni moja ya mikakati ya Bodi ya Filamu inayoitekeleza katika kuendeleza na kuboresha Tasnia ya Filamu katika kada zote hususan Utayarishaji, Uigizaji, Uongozaji na Uhariri wa kazi za Filamu na Michezo ya kuigiza nchini.