Habari
BODI YA FILAMU TANZANIA YAZIDI KUFUNGUA MILANGO YA FURSA ZA KIMATAIFA KWA WADAU WA FILAMU NCHINI.

Serikali kupitia Bodi ya Filamu Tanzania imeendelea kuwa kiunganishi baina ya wadau wa Filamu nchini na wadau kutoka nje ya Nchi.
Tarehe 14 Aprili, 2022 Bodi imewakutanisha wadau wake hususan Watayarishaji, Waongozaji, Waandishi wa Miswada, na mdau wa Filamu kutoka Nchini Marekani (Hollywood) Bw. Wilmot Allen.
Bw. Wilmot alieleza kuwa, yeye pamoja na Wafanyakazi wenzake kutoka Hollywood wameanzisha Maabara ya Kimataifa ya Uandishi ili kusaidia Waandishi wa Filamu na vipindi vya Televisheni kutoka Barani Afrika kutayarisha kazi zao katika viwango vya Kimataifa na kuoneshwa kwenye Televisheni za Marekani.
Lengo la Mkutano huo ni kuwataarifu Waandishi wa Filamu na vipindi vya Televisheni Nchini kuhusu uwepo wa fursa ya kuwasilisha Miswada (Scripts) ya kazi zao kwa Mawakala wa nchini Marekani ili Miswada hiyo ikashindanishwe na Miswada itakayoshinda, itafadhiliwa kwa ajili ya kutayarisha kazi husika, ambapo kazi hizo zitaoneshwa katika Televisheni za Marekani (Hollywood).
Mradi huo ulianzishwa mwaka 2021 na Kenya ilikuwa Nchi ya kwanza kunufaika. Tanzania utekelezaji wake utaanza rasmi Januari, 2023 ambapo utaratibu wa namna ya kushiriki utatangazwa baadae mwaka huu.
Pamoja na mambo mengine, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo alitoa rai kwa Bw. Wilmot kuzingatia Miswada ya lugha ya Kiswahili kwasababu hadithi zetu zinakuwa na maana zaidi zinaposimuliwa kwa lugha ya Kiswahili tofauti na lugha ya Kingereza ambayo inatakiwa kutumika katika uwasilishaji wa Miswada kwenye Mradi huo.
Kwa upande wake Raisi wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) Bw. Eliya Mjatta aliipongeza Bodi ya Filamu kwa kuendelea kufungua milango ya Kimataifa kwa wadau wa Filamu nchini na aliwataka wadau hao kutumia vizuri kila fursa inayojitokeza ili Sekta ya Filamu izidi kupaa Kimataifa na kuitangaza Tanzania.
Taarifa zaidi kuhusu Mradi huo zinapatikana kupitia tovuti ya "WWW.IWLAFRICA.COM"