emblem

Bodi ya Filamu Tanzania

Tanzania: Mandhari nzuri kwa Utayarishaji wa Filamu

Habari

​BODI YA FILAMU NA WALL IS SCREEN KUSHIRIKIANA KATIKA MAFUNZO NA KUONESHA FILAMU DAR ES SALAAM


Katika kuendelea kuimarisha Sekta ya Filamu na Michezo ya Kuigiza nchini, tarehe 12 Disemba, 2023 Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo amekutana na jopo la Wataalamu wa Filamu kutoka Humburg nchini Ujerumani Taasisi ya A Wall is A Screen lililoongozwa na Taasisi ya Ajabu Ajabu Audio Visual kwa lengo la kupanga ushirikiano katika utoaji wa mafunzo kwa wadau wa Filamu nchini ya namna ya kuratibu maonesho ya Sinema katika maeneo ya wazi.

Aidha, mafunzo hayo yatatolewa kwa ushirikiano wa Taasisi ya A Wall is A Screen, Bodi ya Filamu Tanzania, Kituo cha Utamaduni cha Ujerumani (Goethe Institut), pamoja na Taasisi ya Ajabu Ajabu Audio Visual, ambapo yatafanyika kuanzia tarehe 14 hadi 16 Disemba 2023 katika ofisi za Kituo cha Utamaduni cha Ujerumani (Goethe Institut).

Pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo yatafungwa na utazamaji wa Filamu za Ujerumani na Tanzania, katika kuta za majengo ya kihistoria yaliyopo Kisutu jijini Dar es Salaam (Kuta ni Sinema) na baada ya hapo Wataalamu kutoka Ujerumani, pamoja na washiriki wa mafunzo watahudhuria kilele cha Tuzo za Filamu Tanzania 2023 kitakachofanyika katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.