Habari
BODI MPYA YA WAKURUGENZI YA BODI YA FILAMU TANZANIA YAFANYA KIKAO CHA KWANZA

Kufuatia uteuzi wa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Filamu Tanzania Tarehe 25 Machi, 2022 na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa, Tarehe 29 Juni, 2022 Bodi hiyo mpya imekutana na kufanya Kikao cha kwanza ambacho ni Mkutano wa 47 wa Mikutano ya Bodi ya Filamu iliyowahi kufanyika.
Kikao hicho kimeongozwa na Mwenyekiti wa muda Bw. Kenneth Kasigila kutokana na kutokuwepo kwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo Marehemu Profesa Frowin Nyoni aliyefariki dunia kipindi kifupi baada ya kuteuliwa.
Pamoja na mambo mengine, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu ambaye pia ni Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi Dkt. Kiagho Kilonzo aliwapitisha Wajumbe katika ajenda mbalimbali zikiwemo, taarifa ya Bodi na utekelezaji wa kazi zake kwa mwaka wa Fedha 2022/2023, taarifa za miradi mbalimbali inayotekelezwa na Taasisi, taarifa ya Bajeti ya Bodi kwa mwaka wa Fedha 2022/2023, pamoja na Mpango wa manunuzi wa Mwaka wa Fedha 2022/2023.
Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Filamu Tanzania inaongozwa na Mwenyekiti (mchakato wa kumpata bado unaendelea) kwa kushirikiana na Katibu ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo, ambapo inaundwa na Wajumbe watano wakiwemo:-
1. Bw. Kenneth Davis Kasigila - Mratibu wa Miradi wa Benki ya CRDB;
2. Dkt. Mona Mwakalinga - Mhadhiri Mkuu Idara ya Sanaa Bunifu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM);
3. Bi.Leah Elias Kihimbi - Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Sanaa (WUSM);
4. Bw. Salum Abdul Mchoma - Muigizaji, Muongozaji wa Filamu na Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Tanzania (TDFAA); na
5. Bw. Jacob Steve Mbura - Muigizaji na Mtayarishaji wa Filamu.