emblem

Bodi ya Filamu Tanzania

Tanzania: Mandhari nzuri kwa Utayarishaji wa Filamu

Habari

WADAU WA FILAMU KUNUFAIKA NA MAFUNZO YA NAMNA YA KUOMBA UFADHILI WA KUANDAA FILAMU


Kufuatia changamoto zinazojitokeza mara kadhaa katika kuomba ufadhili wa uandaaji wa Filamu kupitia Mashirika ya Kimataifa, Bodi ya Filamu Tanzania imeratibu na kutoa mafunzo maalum ya namna bora zaidi ya kuandaa andiko la mradi ili kuwasilisha maombi ya ufadhili katika mfuko wa maendeleo ya Filamu wa DW Akademie kutoka nchini Ujerumani.

Mradi wa DW Akademie ulianzishwa kwa lengo la kuinua waandaaji wa Filamu wa nchi za Tanzania, Uganda na Ethiopia, ambapo awamu ya kwanza ilinufaisha washindi watano kutoka kila Nchi. Aidha, Dirisha la kutuma maombi ya ufadhili la awamu ya pili la mradi huo limefunguliwa kuanzia Septemba 18, 2022 na litafungwa Oktoba 26, 2022 ambapo wadau wa Filamu nchini wanaweza kutumia fursa hiyo kuomba.

Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza kutolewa Septemba 27, 2022 na yamehusisha Wadau wa Filamu waliofanikiwa kuingia katika kumi bora ya mradi wa maombi ya udhamini (unaotolewa na Bodi ya Filamu) wa Filamu za kimkakati zenye lengo la kuelezea upekee wa Utamaduni wa Watanzania.

Sambamba na hayo, mafunzo yameshirikisha Viongozi wa Chama cha Waandishi wa miswada na Chama cha Waongozaji. Aidha, Mkufunzi wa mafunzo Bw. Hatibu Madudu ni mmoja ya wanufaika waliofanikiwa kupata ufadhili wa mradi huo kwa awamu ya kwanza kutoka nchini Tanzania.