emblem

Bodi ya Filamu Tanzania

Tanzania: Mandhari nzuri kwa Utayarishaji wa Filamu

Habari

TUNATAKA KUIAMINISHA DUNIA KUWA TANZANIA NI KITOVU CHA FILAMU BORA.


Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo alipofanya ziara ya kutembelea Watayarishaji wa Tamthilia ya SINIA wakati wakiendelea na utayarishaji wa kazi hiyo, Tarehe 14 Aprili, 2022 Mwenge jijini Dar es Salaam.

"Lengo la Serikali kupitia Bodi ni kubadilisha mtazamo uliopo sasa kuwa Tanzania hatuna Filamu bora hali inayopelekea Filamu zetu kununuliwa kwa gharama ndogo tofauti na Nchi zingine, hivyo ndio maana nimekuwa nikitembelea wadau kila wakati ili kuona mazingira halisi ya utendaji kazi na kufahamu namna bora ya kutatua changamoto zilizopo" alisema Dkt. Kilonzo

Aliendelea kusisitiza kuwa, Serikali imeweka mazingira wezeshi ya ufanyaji kazi, hivyo ni jukumu la kila mdau wa Filamu katika eneo lake kuongeza umakini na nidhamu ya kazi yake ili kukuza na kulipa heshima eneo hilo.

Alitoa rai kwa Waongozaji wa Filamu nchini kuacha kufanya kazi na wadau wa Filamu ambao hawathamini au kuheshimu kazi zao kwani wanashusha hadhi ya Filamu zetu, badala yake wafanye kazi na wadau makini bila kujali ukubwa au udogo wa majina yao ili kutengeneza thamani ya Sekta ya Filamu.

"Msanii hata awe mkubwa kiasi gani, kama hatopewa kazi basi ukubwa wake hautakuwa na maana, wapeni kazi Vijana wengine ambao hawana majina lakini wana nidhamu ya kazi na wanafanya kazi vizuri" alisema Dkt. Kilonzo.

Akijibu moja ya maswali aliyoulizwa, Dkt. Kilonzo pamoja na mambo mengine, aliwashauri wadau hao kuwa na utaratibu wa kupata taarifa sahihi kuhusu Bodi na Sekta nzima ya Filamu kutoka katika vyanzo sahihi vya Bodi ya Filamu hususan Mitandao yake ya Kijamii na Tovuti "WWW.FILMBOARD.GO.TZ" tofauti na kupata taarifa zisizo sahihi kutoka kwa watu wasio sahihi.

Kwa upande wake Bw. Steven Charles Almasi almaarufu Dkt. Almasi aliwaeleza wadau wenzake umuhimu wa Kitambulisho cha Bodi ya Filamu katika utekelezaji wa majukumu ya Sanaa.

"Mdau wa Filamu lazima uwe na Kitambulisho kutoka Bodi ya Filamu, Kitambulisho ni kinga yako kama Msanii, nilipata shida nilipotaka kusafiri nje ya Nchi kabla sijapata Kitambulisho, lakini sasa Kitambulisho kinanisaidia sana" alisema Dkt. Almasi.