emblem

Bodi ya Filamu Tanzania

Tanzania: Mandhari nzuri kwa Utayarishaji wa Filamu

Habari

KONGAMANO LA WADAU WA FILAMU NCHINI (SYMPOSIUM)


Bodi ya Filamu Tanzania imewakutanisha wadau wa Filamu nchini kwa upande wa Waandaji wa maudhui na Wanunuzi wa maudhui hayo, ambao ni Viongozi wa Makampuni yanayonunua na kuonesha maudhui ya Filamu na Tamthilia za Kitanzania,. Kampuni hizo ni DSTV, AZAM na STARTIMES na Kongamano hilo lililenga kujadili ufumbuzi wa hali ya soko la Filamu na Tamthilia nchini.

Katibu Mtendaji wa Bodi hiyo Dkt. Kiagho Kilonzo amesema Kongamano hilo ni matokeo ya vikao mbalimbali ambavyo Bodi imekuwa ikivifanya kwa nyakati tofauti na wadau hao, hivyo ikionekana haja ya kuwakutanisha pamoja ili pande hizo mbili zijadiliane namna bora zaidi ya utendaji kazi kwa faida ya Sekta nzima ya Filamu na Michezo ya Kuigiza nchini.

Masuala mbalimbali yalijadiliwa ikiwemo uboreshaji wa kazi za Kitanzania hususan katika hadithi ili ziwe na ushindani wa Soko la ndani na nje ya Nchi, Wadau kujiendeleza Kitaaluma ili kuongeza maarifa ya utayarishaji wa kazi bora, pamoja na kutayarisha Filamu kwa kutumia maudhui mazuri yanayoakisi Tamaduni za Kitanzania ili kutangaza nchi yetu na kuepuka kuiga baadhi ya Tamaduni za nchi nyingine ambapo hiyo itasaidia ukuaji wa Soko la Filamu zetu Kimataifa.

Katika hatua nyingine, benki ya CRDB ilishiriki kwenye Kongamano hilo na kuwaeleza wadau hao fursa mbalimbali za uwekezaji zinazotolewa na benki hiyo ambapo wadau wa Filamu wanaweza kunufaika nazo ikiwemo kupata mikopo kwa watakaokidhi vigezo.

Kongamano limefanyika Tarehe 22 Mei, 2022 katika ukumbi wa Makao Makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam.

Tanzania Census 2022